Sunday, 2 February 2014

YANGA YAICHAPA 1-0 MBEYA CITY NA KUVUNJA REKODI YA MBEYA CITY KUTOFUNGWA



Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara timu ya Young Africans leo imevunja mwiko wa timu ya Mbeya City kucheza michezo ya Ligi bila kufungwa baada ya kuichapa bao 1-0 katika mchezo uliofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Kwa ushindi huu wa leo Young Africans wamevunja mwiko wa timu ya Mbeya City kucheza michezo 16 bila kufungwa na kuifanya timu hiyo kutoka jijini Mbeya kuonja shubiri kutoka kwa vijana wa mitaa ya Twiga/Jangwani.

Mchezo wa leo ambao ulivuta hisia za wapenzi na wadau wa soka kwa ujumla, ulikua na mwamko mkubwa kwani wapenzi waliojitokeza kuona mpambano huo na kutaka kushuhudia nani anaibuka na ushindi katika mchezo huo.

Young Africans ambayo leo ilikuwa inacheza mchezo wake wa tatu wa Ligi Kuu chini ya kocha mholanzi Hans Van Der Pluijm iliuanza mchezo kwa kasi kwa lengo la kuhakikisha inapata mabao ya haraka ili kuweza kujitengenezea mazingira ya ushindi.

Dakika 15 za kwanza washambuliaji wa Young Africans Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa na Saimon Msuva walishindwa kutumia nafasi walizopata baada ya kuwa na papara katika umaliziaji na kufanya lango la Mbeya City kuokoa mashambulizi hayo.

Mrisho Ngasa aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 16 ya mchezo baada ya kugongeana vizuri na kiungo Haruna Niyonzima na David Luhende kabla ya Ngasa kumtaza mlinda mlango wa Mbeya City David Burhani na kuukwamisha mpira wavuni.

Young Africans iliendelea kulishambulia lango la Mbeya City na kupata nafasi kadhaa za kufunga lakini umaliziaji wa washambuliaji wake haukuwa mzuri hali iliyopelekea walinzi wa Mbeya City kuokoa hatari hizo.

Mbeya City walifanya mamshambulizi langoni mwa Young Africans lakini umakini wa walinzi wake wa kati Cannavaro na Yondani ulikuwa kikwazo kwao huku Deogratias Munish "Dida" akiokoa michomo ya hatari kati yake na washambuliaji wa Mbeya City.

Mpaka dakika 45 za kpindi cha kwanza zinamilizika, Young Africans 1 - 0.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mashambulizi ya haraka haraka kwa lengo la kupata mabao ya mapema lakini umakini wa walinzi wa timu zote ulikuwa kikwazo kwa washambuliaji hao.

Timu zote zilifanya mabadiliko lakini hayakuweza kubadilisha matokeo ya mchezo, kwani waliendelea kushambuliani na Young Africans kukosa mabao matatu ya wazi kupitia kwa Hamis Kiiza na Saimon Msuva.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 1 - 0.

Kocha Mkuu wa Young Africans mholanzi Hans Van Der Pluijm amewapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa kufuata maagizo yake hali ilyopelekea kuweza kupata ushindi huo ambao umeifanya timu kukaa nafasi ya pili kwenye msimamo na kuwaacha Mbeya City kwa tofauti ya pointi 4 wakiwa nafasi ya tatu.

Mara baada ya mchezo wa leo, kikosi cha Young Africans kitapumzika kesho siku ya jumatatu kabla ya siku ya jumanne kuanza mazoezi kujiandaa na mchezo wa Klabu Bingwa barani Afrika dhidi ya timu ya Komorozine de Domoni siku ya jumamosi.

Young Africans: 1.Dida, 2.Mbuyu Twite/Juma Abdul, 3.Oscar Joshua, 4.Nadir Haroub "Cannavaro", 5.Kelvin Yondani, 6.Frank Domayo "Chumvi", 7.Saimon Msuva, 8.Haruna Niyonzima, 9.Didier Kavumbagu/Hamis Kiiza, 10.Mrisho Ngasa, 11.David Luhende

Mbeya City: 1.David Burhani, 2.John Kabanda, 3.Hassan mwasapili, 4.Deogratias Julius, 5.Yusuf Abdallah, 6.Anthony Matogolo, 7.Mwigane Yeya, 8.Steven Mazanda, 9.Paul Nonga/Richard Peter, 10.Peter Mapunda/Stephen Wilson, 11. Deus Kaseke/Saad Kapanga

No comments:

Post a Comment