MECHI ya mwisho ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara iliyozikutanisha Azam FC na Mbeya City na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3, si tu ilitoa matokeo ya kushangaza lakini imemwachia kilio John Bocco maarufu Adebayor.
Bocco aliumia goti la kulia katika mchezo huo uliochezwa Novemba 7, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam. Timu hizo zilikuwa zikiwania kushika usukani wa ligi hiyo, lakini sare hiyo iliwafanya wafikishe pointi 27 na kushika nafasi ya pili kwa Azam na ya tatu kwa Mbeya City. Matokeo ya mechi hiyo iliyokuwa gumzo yameshaanza kufutika midomoni mwa mashabiki, lakini Bocco bado anaugulia maumivu ya goti lake na hawezi kucheza mechi za mwanzo za mzunguko wa pili.
Awali Bocco aliumia goti hilo mapema mwaka jana katika moja ya mechi za ligi na uongozi wa Azam ulimpeleka India kufanyiwa upasuaji na aliporejea alicheza mechi chache kabla ya kuumia tena.
Bocco alijisikia vizuri baada ya kupata matibabu siku chache baada ya mechi dhidi ya Mbeya City, lakini mechi dhidi ya Zimbabwe ambayo Taifa Stars ilicheza ndiyo iliyotonesha tena goti hilo na hadi sasa anasikilizia maumivu yake.
Baada ya mechi hiyo iliyochezwa Novemba 19 mwaka jana ikiwa ni ya kirafiki kufuata kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) iliisha kwa suluhu na tangu wakati huo Bocco hajawa fiti kupambana uwanjani.
Dakika 80 kwa siku
Mtaalamu wa tiba mbadala, Vincent James ndiye anayemtibu Bocco kwa kumfungia mashine maalumu katika goti lake mara mbili mpaka tatu kwa siku huku kila kipindi akiwekewa kwa dakika 40.
Mashine anayofungwa Bocco inaitwa HiTop PowerStim 142 ambayo inafanya kazi mbalimbali katika viungo vya mwili wa binadamu lakini kubwa ikiwa ni kuvishtua viungo kurudi katika hali ya kawaida.
Kwa mshambuliaji huyo mashine hiyo imefungwa kwenye goti lake la kulia maalumu kwa ajili ya kuiamsha misuli yake iweze kukunjuka na kufanya kazi kama awali.
“Mashine hii inafanya kazi ya kuifanya misuli ya goti kuamka na kuufanya mzunguko wa damu uende kama kawaida, huyu ni majeruhi, ina maana misuli yake haifanyi kazi ipasavyo hivyo mashine hii inaishtua,” anasema Vincent.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, Bocco anafungiwa mashine hiyo kila siku kwa wiki mbili kuendana na ratiba ya mazoezi ya kocha. Wikiendi ndiyo anamaliza kupewa huduma hiyo kabla ya kuruhusiwa kurudi uwanjani kwa ushindani ingawa sasa anafanya mazoezi mepesi huku akimudu kupiga pasi fupi fupi.
No comments:
Post a Comment