Sunday, 5 January 2014

ANASWA KWA KUKODISHA BUNDUKI KWA MAJAMBAZI







MTU mmoja, Taratibu Hemedi (74) ambaye ni mmiliki wa bunduki aina ya shotgun na mwanaye Hemedi Taratibu (32) wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za kukodisha silaha hiyo kwa majambazi.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, ACP Costantine Massawe alisema hivi karibuni kuwa watu hao walikamatwa baada ya watu watano wanaodhaniwa ni majambazi kukamatwa na polisi wilayani Korogwe mkoani Tanga kwa tuhuma za kukutwa na bunduki hiyo na sare za polisi wakati wakijiandaa kwenda kufanya uhalifu .


Kamanda Massawe alisema majambazi hao walikamatwa Kijiji cha Gomba, Kata ya Makuyuni, Korogwe Desemba 28 mwaka jana saa 4:00 usiku baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema.


“Bunduki hiyo ilikuwa na risasi tatu, ina namba ya Model-1400 MK II ambayo Taratibu Hemed ndiye anayeimiliki kihalali, lakini amekuwa akiikodisha kwa majambazi na kuletewa fedha anazotumia kulipia kibali cha umiliki wa silaha hiyo,” alisema Kamanda Massawe.


Aliwataja watuhumiwa hao wa ujambazi kuwa ni Zacharia Jeras (50) Mkazi wa Makanya Same Kilimanjaro, Mosses Jonasi (44) na Selemani Jaha (21) wote wakiwa ni wakazi wa Makanya Same mkoani Kilimanjaro.

Alisema katika mahojiano na polisi walikiri kwenda kufanya uhalifu katika kijiji hicho cha Gomba.
Kamanda aliongeza kuwa polisi inaendelea na uchunguzi ili watuhumiwa waweze kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

No comments:

Post a Comment