Saturday, 28 December 2013

WABUNGE WATATU WA CCM AMBAO NI WAUZA UNGA WAJISALIMISHAA





Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste, William Mwamalanga


Baada ya tishio la kupelekwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC, watu watano wakiwemo wabunge watatu wa CCM wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya wamejisalimisha kwenye kamati ya kidini inayojihusisha na maadili nje na ndani ya makanisa.

Katika mahojiano maalum na NIPASHE Mwenyekiti wa Kamati ya maadili na haki za binadamu kwa jamii nje na ndani ya madhehebu ya dini, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste, William Mwamalanga, alitoa taarifa hizo.

Alieleza kuwa wabunge hao (majina yanahifadhiwa) ni wa viti maalum kutoka mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam na Mara.

Alisema mbali ya wabunge wamo viongozi wa dini na mfanyabiashara maarufu ambaye alikuwa akisafirisha mihadarati mkoani Mbeya.

Mchungaji huyo alisema kujisalimisha huko kunatokana na kamati hiyo mwezi Oktoba mwaka huu kuwataka vinara 61 wakiwemo wabunge hao kujisalimisha kwa ridhaa zao kwa Rais Jakaya Kikwete kama njia ya kutubu makosa yao.

Kinyume na hapo kamati hiyo iliweka wazi uamuzi uliofikiwa kuwa ni kuwapeleka watu hao katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iliyoko jijini Hague nchini Uholanzi ili sheria kuchukua mkondo wake.

Mchungaji Mwamalanga alisema kamati ilitoa muda wa miezi miwili ambayo inaisha mwezi huu.

Alisema kutokana na ukaidi huo majina ya watu 56 ya wale ambao hawajajisalimisha ifikapo Januari 15 mwakani yatakabidhiwa rasmi kwenye taasisi za kupambana na dawa za kulevya Umoja wa Mataifa ili wafikishwe ICC.

“Novemba 15, mwaka huu tuliyaingiza majina 61 kwenye mtandao wa taasisi hizo, baada ya hawa watano kuja kwetu, tulipeleka mrejesho kwa taasisi hizi kuwa tumewatoa ingawa nao hawakuenda kwa Rais,” alisema na kuongeza:

“Baada ya kuyaingiza majina haya kwenye taasisi hizi, uchunguzi wa taasisi hizi ulibaini watu hawa ni kweli wanajihusisha na biashara hii, sasa tunachofanya hivi sasa ni kuyakabidhi majina ya wale waliokaidi ili hatua zaidi ziweze kuchuliwa,” alisema.

Alisema kwa sasa kamati ipo katika hatua ya mwisho ya kufanya kazi ya kukusanya majina ya watu waliofariki kwa dawa za kulevya nchini kama ushahidi kwenye kesi hiyo.

Alisema majina hayo wanayakusanya kupitia kwenye hospitali na kwa ndugu wa marehemu waliofariki kutokana na dawa ya kulevya.

Alitaja baadhi ya takwimu walizokusanya za vifo vya baadhi ya watu waliofariki na dawa hizo kwenye mikoa na wilaya kuwa ni Mbeya 38, Kinondoni 67, Dodoma 19, Tanga 41, Lindi saba.

Mchungaji Mwamalanga alisema baadhi ya takwimu hizo ni za mwaka mmoja na nyingine miaka mitatu iliyopita.

Aliongeza kuwa wanaendelea na zoezi la kukusanya takwimu hizo kwenye maeneo mengine.

Kuhusu wale waliojisalimisha kwao ambao gazeti hili inayo majina yao, Mchungaji huyo alisema kamati imewawekea ulinzi wa siri wa kuifuatilia mienendo yao ili kubaini kama wameacha au la kama walivyokiri kwao.

Mchungaji Mwamalanga, alisema moja ya masharti waliyotoa kwa watu hao watano ni kutoa ushirikiano utakaowezesha kukamatwa wale wanaoendelea na kuingiza au kusafirisha nje ya nchi dawa hizo.

Alisema tayari watu hao wameshatoa ushirikiano na kuwezesha kukamatwa watu kadhaa waliokuwa wakisafirisha dawa hizo kwenda nchi nyingine duniani.

Alisema watu hao waliwatajia mbinu ambazo hutumika kusafirisha dawa hizo kuwa ni baadhi wamekuwa wakizihifadhi kwenye ‘uume bandia’ na kwenye midoli.

“ Walitueleza kuwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki na zile za Maziwa Makuu, wafanyabiashara wamebadilisha mbinu za usambazaji wa dawa hizi ambapo njia hizo ndizo hutumika, ukimuona mwanamke kabeba mdoli wengine huwa wamebeba dawa hizi,” alisema.

Pia alisema watu hao waliwaeleza mbinu nyingine ni dawa kusafirishwa kupitia kwa baadhi ya wafadhili wanaoshughulika na mambo ya afya.

Mchungaji Mwamalanga amewaasa vinara hao kuzitumia sikukuu za mwisho wa mwaka huu kujisalimisha wenyewe ili ifikapo mwakani taifa liache kuzungumzia suala hilo.

“Tunawaomba wajisalimishe wenyewe, wanadhani sisi tunafanya mzaa lakini tunawaambia kuwa, watekeleze yale tuliyowataka,” alisema.

Mkutano ambao uliibuka na maamuzi ya kuwafikisha vinara hao ICC ulifanyika siku mbili kuanzia 21 Oktoba mwaka huu na kuhudhuriwa na viongozi wa dini wa madhehebu ya Kiislam na Kikristo 134 kutoka Bara na Visiwani.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment